Jitambue Ya Chris Mauki.......ITAMBUE HAIBA YAKO (Know your Personality)
Katika
utafiti wakuchunguza athari za msongo wa mawazo katika moyo, madaktari
Mayer friedman na Ray Roseman waliweza kuwaweka watu katika makundi ya
haiba mbili; yaani haiba kundi A and haiba kundi B.
Madaktari
hawa waligundua kuwa hata kama kazi na aina ya maisha ingefanana, watu
wa haiba kundi A wangekuwa na nafasi mara 3 kuteseka na msongo wa
mawazo, magonjwa ya moyo, shinikizo la damu n.k. na watu hawa mara
nyingi huwa wanamaudhi kwa jinsi wanavyojibu au kuongea na wengine, na
hili limekuwa likiwaongezea msongo wa mawazo maradufu.
Makundi
haya yamewekwa ili kukuwezesha wewe kujua uko upande gani.
Usichanganyikiwe wala kushtuka pale utakapojikuta una tabia za makundi
yote mawili, mara nyingine inaamaanisha kuwa uko vizuri katika
kuhakikisha mambo yanafanyika inavyotakiwa au unavyotaka yawe. Ila kama
unajikuta unatabia zaidi ya nusu za haiba kundi A inabidi uchukue uamuzi
wa kutafuta kubadilika au kubalisha mtazamo ulionao katika maisha,
kabla haujajihatarishia maisha yako wewe mwenyewe.
Haiba Aina ‘A’
- Ni watu wa ushindani katika kila kitu wafanyacho.
- Watu wenye haiba ya kutumia nguvu na kulazimishisha
- Hufanya mambo yao mengi kwa haraka
- Huwa na uchu wa kupandishwa vyeo na kujulikana katika jamii. (Hatakama hawana sifa).
- Hutaka sana kujulikana na kuheshimiwa kwa kile walichokifanya.
- Hukasirishwa kwa haraka na watu au matukio fulani
- Huongea mara kwa mara kwa kufoka au kwa vitisho
- Hupenda kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja.
- Hutembea na hata kula kwa haraka
- Mara nyingi kuchukizwa sana pale wanapocheleweshwa
- Hujali sana muda na kukazana kumaliza mambo kwa muda ulipangwa (meating deadlines)
- Kila mahali huwepo kwa wakati na kwa muda muafaka.
- Mara kwa mara misuli yao ya uso huonyesha, kumaanisha, kuogopesha au ukali,
Haiba Aina ‘B’
- Sio watu wa ushindani mfano, makazini, michezoni, masomoni n.k.
- Ni watu walio rahisi, na huyakubali mazingira, hufanya vitu taratibu na kwa kufuata kanuni.
- Huendelea na kuchukuliana na hali ya kazi iliyopo.
- Huridhika na nafasi walinayo katika kijamii.
- Hawahitaji kujulikana au kutambulika katika jamii au hata katika matukio.
- Sio rahisi sana kuwaudhi.
- Mara nyingi hufurahia sana wanapokuwa pekeyao.
- Ni wavumilivu.
- Hupendelea kufanyakitu kimoja kwa muda muafaka kabla ya kwenda kwenye kitu kingine.
- Hutembea, na kula kwa nafasi na utulivu.
- Hawakimbizwi sana na muda, sio wakukimbizana sana na kumaliza kazi.
- Mara nyingi ni wachelewaji.
- Nyuso zao ni za kufurahi na sio za mikunjo.
KWANINI UKO VILE ULIVYO?
Vyovyote
haiba yako ilivyo na kwa vyovyote unavyowachukulia wenye wale tabia
ngumu fahamu kuwa mfano huo ulishakuwepo miaka mingi iliyopita, labda
zaidi ukiwa mtoto ndio ilikuwa chanzo cha vile ulivyo leo;
Mwanasaikolojia mmoja aliuita mfumo huu..“A child is a father of a man” yaani
Mambo
tunayoyaona au unayoyaona kwa mtoto hutupa picha halisi ya ukumbwa wake
utakavyokuwa. Zaidi ya asilimia sitini ya yote yanayoendelea maishani
mwetu leo yanachangiwa na makuzi yetu tukiwa watoto
Wengi
wetu tumejiharibia misingi yetu ya uwezo wa kuishi na watu wenye tabia
ngumu na hivyo kujikuta tunaumizwa tokea tukiwa watoto wadodo. Habari
njema ni kwamba hakuna ulazima wa kubaki vile ulivyo, mabadilko
yanawezakana, inawekana katika hatua yoyote kubadili mtazamo au
muonekano wako na kuboresha ujasiri wako.
Tujaribu
kuangalia baadhi ya sababu zinazosababisha mtu kujiona au kujitazama
vibaya, hii itakuwezesha wewe kujua uko wapi na kwanini.
- Watu wa kwanza kabisa waliowahi kuwa karibu na wewe ni baba na mama yako au yoyote aliyechukua nafasi yao, mfano mlezi, babu, bibi nk. Kutokana na mtazamo wao juu yako, hapo wewe umetengeneza au kuzalisha mtazamo juu yako mwenywe najinsi unavyojithamini au kutojithamini. Kwa lugha rahisi ni kwamba, jinsi unavyojiangalia ulivyo leo kunatokana kwa kiasi kikubwa na jinsi wao walivyokuwa wanakutazama, kama walikuona wewe lofa na mjinga basi kuna uwezekano mkubwa na wewe leo utajiona lofa tu.
Najua
wapo wazazi wasio na hekima wala wema kwa watoto wao, huwasababishia
watoto wao majeraha ya kimwili, kihisia na hata kiakili, uzuri ni kwamba
fungu la wazazi hawa ni dogo. Ingawa inawezekana sana kwa wazazi au
walezi au watu wazima wowote kusababisha majeraha na athari kwa watoto
mara nyingine pasipo kujua kwamba wanafanya hivyo. Katika kuongea na
wazazi lukuki nimegundua kwamba asilimia kubwa ya watoto wameharibiwa na
wazazi wao wenyewe, pasipo wazazi hawa kujua kuwa wanawaharibu watoto
wao.
- Wazazi ambao huwalinda na kuwatetea sana watoto wao, wakijaribu kuwafanyia kila kitu kwa niaba ya watoto hao, kwa njia hii wazazi hawa hutengeneza watu wazima (wababa au wamama) wenye utegemezi mkubwa, wasioweza kufanya kitu chochote wenyewe wala kusimama kwa miguu yao wenyewe. Unakuta hata kazi za shuleni mama ndiyo anafanya, mtoto anakuwa hata kuosha mwili wake hajui, na hawa ndio wale ambao ndoa huwashinda mapemaaa.
- Wale wazazi au walezi ambao hutoa mahitaji kwa watoto wao lakini hushindwa kuonyesha kwa matendo upendo wao kwa watoto wao (mfano. Kuongea nao, kucheka nao, kucheza nao n.k.) hutengeneza kizazi kinachoamini kuwa hakipendeki, hakina mvuto, kisicho na thamani na kisichostahili kupendwa. Baba haijalishi unatoa mahitaji yote yanayohitajika nyumbani kwako, hilo sio pekee watoto wako wanalolihitaji kutoka kwako, wape muda wakuwa pamoja nao, waruhuru kucheza na wewe kidogo, toka pamoja nao, jibu baadhi ya maswali yao, waruhusu kujuwa kumbe baba au mama anaweza kuwakaribu na sisi pia.
- Wazazi au walezi ambao kila mara humwekea mazingia mtoto kujiona aliyeshindwa, kila wakati ni wakufeli tu, wazazi hawa ni wale wanaosema kwa nini mtoto asijitahidi, kwanini asiwe wa kwanza darasani, ni mpumbavu n.k.. hali hii huharibu kabisa imani ya mtoto kwake yeye mwenyewe, huua kule kujiamini kwake na pia kutokiamini kile anachokifanya.
Yawezekana
kuna vitu vilivyoonekana katika makuzi ya mtoto ambavyo hakuna wa
kulaumiwa lakini bado vitu hivi huathiri sana kujiamini na kujithamini
kwa mtoto yule.
Mtoto
au watoto wanaohama hama au kuhamishwa shule mara kwa mara, kwa sababu
zao binafsi au kwa sababu ya kuhama hama kwa wazazi hupata shida
yakujiona wapweke kwa maana kila wakati hupata kazi ya kutengeneza
marafiki wapya na kwamuda fulani hali hii huathiri haiba zao na kujenga
kitu tunachokiita “inferiority complex”
Tufanye nini??
Kitu
cha kwanza ni kukubaliana na ukweli kwamba mtazamo wako (jinsi
unavyojitazama) hubadilika badilika. Tena hubadilika kiasi ambacho mara
nyingine huwezi kutambua. Unaweza kuchagua mwenyewe jinsi unavyotaka
mtazamo wako uwe. Kwa mfano;
- Kufanikiwa au kushindwa
Jaribu
kutoangalia nyuma kule ulikowahi kushindwa zaidi, kila mtu anahistoria
ya kushindwa sio wewe tu. Wacheza mpira maarufu duniani, mara nyingine
hukosa magoli rahisi kabisa lakini hakuna hata mmoja aliye acha kucheza
au kuharibu fani yake kwa sababu ya kukosa goli. Wala hakuna aliyekiri
kuwa yeye sio bora kwa sababu tu ya kukosa goli moja. Ni vema kukumbuka
kule tulikowahi kushindwa kama tu tunataka kujifunza katika makosa yetu,
na sio kwa kutaka kujisononesha na kujilaumu kwa namna tulivyokosea. Jifunze kuziacha historia za kufeli na kushindwa zifukiwe katika yaliyopita.
Tengeneza
mafanikio yako wewe mwenyewe anza katika hali ya chini kabisa, chagua
vile vitu usivyo viweza kabisa kuvifanya mfano; Kuzungumza mbele ya
watu, kuimba, kuogelea, kuwa kwenye usaili, kusimama mbele ya kamera n.k
anza kuvifanya kwanza kupitia ufahamu wako (viwaze akilini) hali hii
inaitwa (creative visualization) ni njia majawapo bora ya kufanya
mazoezi ya vile tunavyoshindwa katika fikra zetu, kwanza jitahidi
kujitazama fikrani ukiwa au ukifanya vitu hivyo kwa ushindi hadi ufahamu
wako utakapoizoea hali hiyo na kuacha kutuma jumbe za kushtuka
(kupanick) au uwoga wakati utakapokuwa unafanya vitu vile kihalisi.
Katika
kufanya mazoezi ya kufikiria kimtazamo, chagua kufanya katika utulivu
mchana au jioni. Muda kabla hujaenda kulala ni mzuri zaidi. Rudia zoezi
hili mara kwa mara mpaka uzoee na fikra zizoee.
- Andika vile vitu uvipendavyo juu yako mwenyewe, kama kuna mtu anayesema kuwa hana kitu cha kuandika basi mtuhuyo hajafikiri kwa undani au ni mwongo, kila mtu anakitu chema ndani yake.
Kama
ukishaandika vitu hivi, angalia tabia ya vile vitu ulivyoviandika pale,
kama vitu hivyo vikifanywa na mtu baki usiyemjua je utasema yeye ni mtu
mbaya? Kama sio, kwa nini wewe unajiona usiyefaa na uliyejaa mabaya tu?
Badala
ya kutazama yale yaliyo mabaya na yakushindwa katika historia yako
tazama mafanikio yako. Kila mmoja ana mafanikio ya aina fulani, hata
kama ni madodo kiasi gani. Hata kama unatazama yale yaliyowahi kufanyika
huko awali basi yatazame katika mtazamo chanya.
Wengi
wetu hatuchukui muda kujiuliza vyanzo vya mitazamo yetu hasi, tunaamua
kuikubali tu na kuikumbatia na kuifanya asili yetu. Ila mara tu utakapo
gundua kuwa tatizo sio lako wewe bali ni mazingira uliyokuziwa au aina
ya wazazi uliokuwa nao basi utaacha kujidharau.
Wako
watoto wanaofurahia kupelekwa shule za bweni mbali na nyumbani, ila
wako ambao hawapendi kabisa lakini wanalazimishwa, hali hii hupandikiza
ndani ya watoto hawa upweke, hofu, msongo wa mawazo na kutokutulia
(nazungumzia utulivu wa ndani) jambo ambalo huendelea hata katika utu
uzima wao. Wako wengi ambao tabia zao za leo zilianza kuharibikia katika
shule za bweni mbali na wazazi kwa mfano tabia za kusagana au
kuingiliana kinyume na maumbile.
Sisi
tumeumbwa katika mifumo na vipindi mbalimbali, mara nyingine tuko
chanya (watu wema, wazuri) na mara nyingine tunakuwa hasi (watu wabaya).
Kama mtoto atakuwa akiambiwa kila wakati kuwa “kamwe huwezi kuwa na
akili kama dada yako” maneno haya hufanyika halisi kwake. Je hujawahi
kusikia mtu akisema “mimi sijui kuogelea”, “mimi sijui kama nitaolewa”
“Kamwe sitokaa niendeshe gari” , “Mimi sitokaa nijue kiingereza”, “Mimi
na kuimba ni tofauti” Haimaanishi kama watu hawa wangeanza kujifunza au
kuzaliwa katika mazingira ya vitu hivi, wangevishindwa. Labda kuna
sehemu mtu au watu fulani waliwasemea kutoweza au kushindwa na huo ukawa
mwanzo wa kuwekewa kizingiti cha ujuzi ndani yao.
Wakati
wowote mtu anapojisemea jambo, au neno lililo baya, lisilojenga,
lakushindwa, kama utalisema kwa sauti au utalifikiria akilini, katika
hali yoyote ile jambo hili hulazimisha uhalisi wa maneno yale kuingia
katika mfumo wa maisha yako na kutenda kazi kwa hiyo jifunze kukataa,
kukanusha na jitahidi kutenda kinyume na zile sentensi mbaya juu yako.
Kama tunaamini utendaji wa kazi wa yale tunayojisemea au kusemewa vibaya
basi hata yale tunavyojisemea au kusemewa vema hutenda kazi pia. “If
negative proclamation works, surely positive proclamation must work too”
Amua kubadilisha yale unayojisema au yale unayosemewa. Badili yale
yaliyo negative (yakufeli) yawe positive (yakuweza). Kama hujiamini wewe
mwenyewe wala hujithamini, basi utakubali kirahisi kila neno gumu na
baya utakaloambiwa na kila mwenye tabia ngumu na kama utayakubali
unayoambiwa au unayorushiwa hutaweza kamwe kukabiliana na ushindani
kutoka kwa mtu au watu wenye tabia ngumu. Kumbuka daima udhaifu huanzia
kwako mwenyewe.
Ukishajifunza
kupunguza kujilaumu na kujipinga mwenyewe na kuboresha jinsi
unavyojitazama basi utakuwa salama katika kukabiliana na maneno na
matendo magumu toka kwa yeyote mwenye tabia ngumu. Na kwa kuwa
umejifunza vizuri kujielewa basi sasa waweza kuwaelewa vizuri zaidi wale
wenye tabia ngumu. Sasa utaweza kuelewa kuwa kuna kitu kimemfanya au
kimewafanya wawe vile walivyo. Mara utakapoweza kumwonea huruma yeyote,
haijalishi anatisha kiasi gani basi hawezi tena kukuathiri kwa vyovyote
vile.
Kwa
jinsi ujasiri wako unavyoongezeka, unaweza pia kuziweka katika matendo
mbinu nyingine nyingi za kushuhulika na watu wenye tabia ngumu.
Utajikuta unaweza kukabiliana nao na pia kuchukuliana nao katika
mazingira tofauti na pia hata katika nyakati ambazo hutakuwa unafanya
vizuri katika jambo fulani, hautajilaumu na kujishusha, bali utajisifu
kwa kukazana na kujitahidi hata kama haukubahatika.
Chris Mauki
Social and counselling psychologist
PhD candidate
University of Pretoria
chriss@udsm.ac.tz
No comments:
Post a Comment
YOUR WORMY WELCOME TO SAY ANYTHING TO ME IN MY WEBSITE